
Kumekuwepo taarifa ambazo zimekuwa zikiripotiwa kupitia Vyombo
mbalimbali vya Habari pamoja na mitandao ya kijamii kuwa, Serikali ya
Tanzania inafanya operesheni maalum inayolenga kuwaondoa Raia wa Kenya
wanaoishi nchini bila kuwa na Vibali halali huko Wilayani Longido, Mkoa
wa Arusha, huku wakimhusisha Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu katika utekelezaji
wa ‘zoezi’ hilo.
Taarifa hizi zimezua tafrani na kutishia hali ya usalama iliyopo katika
mpaka wa Tanzania na Kenya, Namanga.Tunapenda kutoa ufafanuzi kuhusu
Taarifa hizo zinazoendelea kuenezwa kuwa:-
1.Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haijafanya operesheni
yoyote inayolenga kuwakamata na kuwaondoa nchini raia wa Kenya au Taifa
lolote lile wanaoishi katika Wilaya ya Longido Mkoani Arusha kama
inavyoenezewa kwenye Vyombo vya Habari na Mitandao mbalimbali ya
kijamii.
2.Shughuli za udhibiti wa raia wa kigeni wanaokiuka Sheria za Uhamiaji
nchini hazifanywi kwa kulenga Taifa lolote lile, bali hufanywa kwa
kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi. Wahusika wanaokiuka Sheria,
Kanuni na Taratibu za uhamiaji hukamatwa na kuchukuliwa hatua kwa makosa
yao binafsi na sio kwa msingi wa utaifa wao.
3.Kukamatwa kwa raia wa kigeni ambao walibainika kuwa ni raia wa Kenya
ni sehemu ya shughuli za kawaida za Idara ya Uhamiaji kama Chombo cha
Ulinzi na Usalama katika kuhakikisha kwamba raia wa kigeni wanatambuliwa
na kuishi kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi.
4.Suala la kukamatwa kwa raia hao wa Kenya ambao walibainika kukiuka
Sheria ya Uhamiaji nchini halihusiani kwa njia yoyote ile na Serikali ya
Tanzania kulenga kuwakamata raia wa nchi yoyote na wala si agizo la
Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kama ilivyoripotiwa, bali ni utaratibu wa kawaida ambao unafanywa na
nchi yoyote katika kuhakikisha kwamba ukaazi wa wageni unazingatia
Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi husika. Kwa mfano, katika mwezi
Februari 2017, Idara ya Uhamiaji imewakamata wageni 396 kutoka mataifa
mbalimbali kwa makosa ya kiuhamiaji na kuwachukulia hatua mbalimbali kwa
mujibu wa Sheria.
5.Tanzania na Kenya tunao uhusiano mzuri sana ambao ni wa kihistoria na
nchi hii ni mwanachama mwenzetu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa
uhusiano huo, wapo watanzania wengi wanaokwenda nchini Kenya kwa sababu
mbalimbali kama vile matembezi, biashara, masomo nk. Pia wapo raia wengi
wa Kenya wanaoingia na kuishi hapa nchini kwa sababu kama hizo hizo na
hatuna tatizo nao, alimradi hawavunji Sheria za nchi yetu.
6.Mwisho, tunatoa wito kwa Wageni wote wanaoishi hapa nchini kwa
shughuli mbalimbali kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za uhamiaji
nchini. Wapo baadhi ya wageni wanaoingia nchini kihalali, lakini
wanaendelea kuishi nchini hata baada ya muda waliopewa kuishi nchini
kumalizika. Aidha, wapo baadhi ya wageni wengine wanaoingia nchini
kinyume cha sheria na kuendelea kuishi nchini kinyume cha Sheria. Wale
wanaobainika kukiuka Sheria, Kanuni na taratibu za uhamiaji nchini
watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria bila kujali utaifa wao.
7.Taarifa zinazoenezwa kupitia Vyombo vya Habari na Mitandao ya kijamii
kwamba Tanzania inawalenga raia wa Kenya, kuwakamata na kuwaondoa nchini
si sahihi na zipuuzwe kwani zinalenga kuchafua na kuzorotesha uhusiano
mzuri uliopo baina ya nchi zetu mbili na wananchi wake, pamoja na
kudhoofisha shughuli za udhibiti wa wahamiaji haramu nchini.
8.Tunafahamu kuwa Tanzania haiwezi kuishi kama kisiwa. Hivyo,
tutaendeleza na kuimarisha ushirikiano na Mataifa mengine pamoja na
kuendelea kuweka mazingira mazuri kwa wageni kuja na kuishi nchini kwa
shughuli mbalimbali, zikiwemo biashara, uwekezaji, utalii, matembezi na
nyinginezo.
Imetolewa na;
KITENGO CHA UHUSIANO,
MAKAO MAKUU, IDARA YA UHAMIAJI,
BARABARA YA LOLIONDO, KURASINI,
S.L.P 512, DAR ES SALAAM.
31 MACHI, 2017.
www.immigration.go.tz