Mwanaharakati wa masuala ya jinsia nchini Tanzania Dkt. Avemaria
Semakafu amemshukuru Rais Magufuli kwa kumteua kuwa Naibu Katibu Mkuu
Wizara ya Elimu huku akiweka wazi kuwa uteuzi huo utamfanya awe kimya
katika harakati zake.
Akizungumza ya simu mara baada ya uteuzi huo kutangazwa, Semakafu
ambaye pia ni Mhadhiri Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi
Muhimbili (MUHAS) ameahidi kuitumikia nafasi hiyo kwa uaminifu na
uadilifu mkubwa, na kwamba kwa nafasi hiyo ni vigumu kuendelea kupigia
kelele masuala mbalimbali kama alivyokuwa anafanya kwa kuwa nafasi hiyo
ina utaratibu wake.
"Sasa hamtanisikia tena, ndiyo nimefungwa mdomo, huku huwa hawaruhusu kuongea". Amesema Dkt. Semakafu.
Dkt. Semakafu anafahamika zaidi nchini kwa kutoa na kuchangia mada
mbalimbali kupitia mihadhara na vipindi vya luninga vinavyohusu mijadala
mbalimbali ya kijamii na kitaifa. Pia alikuwa ni mjumbe katika Bunge
Maalum la Katiba mwaka 2014, wakati huo akiwa mratibu wa Mtandao wa
wanawake na Katiba (Ulingo)
Kuhusu kuendeleza harakati zake, amesema ni vigumu kuzifanya harakati za
jinsia lakini atajitahidi kutumia uwezo wake kusukuma masuala kadhaa
yahusuyo elimu kwa mtoto wa kike kwa ushirikiano na watu atakaowakuta
wizarani, lakini pia kwa kufuata miongozo iliyopo.
"Kwenda wizara ya elimu ni fursa kwangu lakini ifahamike kuwa nakwenda
mahali ambapo tayari kuna mipango ambayo tayari imeshawekwa, kwahiyo ni
kwenda kuangalia changamoto ambazo zimeanishwa na mipango iliyowekwa na
jinsi gani itatekelezeka katika kushughulikia kuzitatua... Nitakwenda
kujifunza na kwa kutumia harakati zangu, waliopo pale pia watajifunza
kwangu" Amesema Semakafu
No comments
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
