ALIYEKUWA Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari, MAELEZO, Raphael
Hokororo ameiambia Mahakama kuwa walimpa taarifa Rais John Magufuli ya
kufungiwa kwa gazeti la Mawio kwa sababu jina lake lilitajwa kuwa mmoja
wa watakaosababisha machafuko Zanzibar.
Hokororo alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam alipotoa ushahidi katika
kesi ya tuhuma za uchochezi dhidi ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu
Lissu, Mhariri wa Mawio, Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa
Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.
Mkurugenzi huyo alidai hivyo wakati akijibu swali la wakili wa
washitakiwa, Peter Kibatala alipomwuliza kama walimpa taarifa Rais
Magufuli baada ya wizara husika kulifungia gazeti hilo, akajibu kuwa
taarifa alipewa kwa sababu jina lake lilitajwa kwenye habari iliyosema
‘Machafuko yaja Zanzibar.
Shahidi huyo alidai hatua hiyo ilifikiwa na Wizara ya Habari Utamaduni,
Sanaa na Michezo baada ya wao kupeleka ripoti kuwa habari iliyochapishwa
na gazeti hilo toleo namba 182 la mwaka jana, ilikuwa na maudhui ya
uchochezi kwa walichodai kuwa Serikali ya Zanzibar inaongozwa na uamuzi
kutoka Tanzania Bara.
Pia alidai kuwa baada ya kichwa cha habari kuwa ‘Machufuko yaja
Zanzibar’ ilielezwa kuwa ‘Magufuli kubeba lawama’ na ‘Zanzibar
inaongozwa Dar es Salaam, Tanzania Bara maana kila kitu kinachoamuliwa
kutoka huko ndicho chanzo kingine cha migogoro Zanzibar’.
Hata hivyo, alidai kuwa baada ya gazeti hilo kufungiwa polisi walikwenda
kuchukua maelezo yake, lakini hajui kama gazeti hilo lilifunguliwa na
Mahakama kwa sababu tayari alikuwa amestaafu.
Ilidaiwa kuwa Januari 12 hadi 14, 2016 Dar es Salaam, washitakiwa Jabir,
Mkina na Lissu, kwa pamoja waliandika na kuchapisha taarifa za
uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’.
Katika mashitaka ya pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 Dar es Salaam,
walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.
Mshitakiwa Mehboob anadaiwa kuwa Januari 13, 2016 katika jengo la Jamana
lililopo Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, alichapisha gazeti la Mawio
lililokuwa na taarifa za uchochezi.
Alidai mshitakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.
Mbali na mashitaka hayo kwa pamoja wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016, Dar
es Salaam, bila mamlaka yoyote, waliwatisha na kuwatia hofu wananchi wa
Zanzibar wasiingie kwenye marudio ya Uchaguzi Mkuu.