RAIS mstaafu wa Awamu ya Pili, Ally Hassan Mwinyi amemuomba kiongozi wa
dini ya Wahindu ya Swaminarayan Duniani, Mahant Swami Maharaji kuiombea
Tanzania amani na umoja viweze kudumu na kusiwepo aina yoyote ya ubaguzi
kwa sasa na hata vizazi vijavyo.
Mwinyi aliyasema hayo Dar es Salaam baada ya kualikwa katika hafla ya
kumkaribisha kiongozi huyo hapa nchini na kukutana na waumini wa dini
hiyo.
Pia ilikua ni maadhimisho ya miaka 40 tangu kujengwa misikiti miwili ya dini hiyo hapa nchini.
Alishukuru kwa kualikwa katika hafla hiyo ya kidini kwani sio jambo la kawaida kupokea ugeni wa kiongozi wa kidini nchini.
“Sina shaka kuwa sio nchi zote wenye kuwa na uwezo wa kumuona kiongozi
mwenye nafasi kubwa kama hiyo katika nchi zote,” alisema na kuongeza
kuwa kama Watanzania wengine amekuwa mwenye bahati.
Alimkaribisha kiongozi huyo nchini na kumtaka kuiombea sana Tanzania ili
iendelee kudumisha amani na umoja na licha ya kutokuwepo kwa aina
yoyote ya ubaguzi, aendelee kuomba ili hali hiyo isiwepo kamwe na
wananchi waendelee kuishi kama ndugu.
Kwa upande wake, kiongozi huyo ambaye ni wa sita kwa nafasi hiyo,
Maharaji alisema ataendelea kuiombea Tanzania na dunia nzima kwa ujumla
ili wananchi wake waendelee kubarikiwa katika maisha yao pamoja na
kukuza maendeleo yao.
Alisema mwanadamu siku zote hupenda raha lakini ni vyema wakafahamu kuwa
hakuna raha kubwa kama kupata kutoka kwa Mungu kwa kuwa raha nyingine
zote ni za muda, hazidumu.
“ Starehe ya mwanadamu ni ya muda mfupi na raha ya kuishi anayeitoa ni
Mungu na ambayo haidumu, hivyo siku zote yapasa kuomba sana kwa Mungu
kupata raha ya kudumu,” alisema na kusisitiza wajibu wa kila mwanadamu
kuomba amani siku zote na kila wakati na kuishi kwa kanuni za Mungu.