Kwa taarifa za uhakika kutoka Dodoma, kupitia kikao cha Kamati ya Kanuni
ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Uchaguzi wa Wabunge wa
Bunge la Afrika Mashariki utafanyika kama ilivyotangazwa na Spika wa
Bunge Mh. Job Ndugai kwa kuzingatia Ibara ya 50 ya Mkataba wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki na Kanuni za Kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Katika kikao chake kilichoketi jana hadi majira ya saa nne usiku,
taarifa hizo zinathibitisha kuwa ombi la KIONGOZI MKUU wa ACT, kutaka
chama hicho kipewe haki na nafasi ya kuweka mgombea uchaguzi wa EALA,
limetupiliwa mbali kwa sababu halikuwa na mashiko ya kimantiki wala
msingi wa kikanuni.
Kiuhalisia kamati hiyo imeungana na Spika Ndugai na kumpongeza kwa
kusimamia kanuni za uchaguzi huo hasa kwa kuzingatia msingi wa Kanuni ya
12 inayosema kuwa Uchaguzi wa EALA utafanyika kwa kuzingatia uwiano wa
vyama vyenye uwakilishi bungeni.
Chama kama ACT chenye mbunge mmoja katika Bunge la lenye idadi ya
wabunge 393 ni sawa na 0.00% ambayo ni sawasawa na kiti au viti 0. Kwa
hiyo taratibu zinakiengua kuwa katika mchakato wa kugombea hata nafasi
moja.
Vile vile kanuni ya 5(5) ya Nyongeza ya Tatu ya Kanuni za Bunge inasema
"chama chochote cha siasa chenye HAKI ya kusimamisha mgombea wa EALA
kinaweza kuweka wagombea watatu katika makundi ya wagombea ubunge."
Mantiki ya hoja kutokana na msingi huo wa kikanuni, inaonesha kuwa vyama
vingine tofauti na CHADEMA, CUF na CCM, haviwezi kusimamisha wagombea
kwa sababu havikidhi kigezo cha Kanuni ya 12 ya Kanuni za Kudumu za
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kimsingi Spika amesimamia haki iliyokuwa inaporwa au kupokwa katika
chaguzi za EALA zilizopita. Kwa uamuzi huo bila shaka sasa uchaguzi
utahusisha vyama vitatu ambavyo ni CCM (6), CHADEMA (2) na CUF (1)
ambavyo ndivyo vinakidhi vigezo vya kuweka wagombea.
Ibara ya 50 ya Mkataba wa wa EAC, inaelekeza na kutoa mamlaka kwa kila
bunge la nchi mshirika kuchagua wawakilishi kwa mujibu wa kanuni za
bunge la nchi husika na huo ndio utaratibu uliopo sasa ambao wapeleka
maombi wanaujua vyema.
Ni wazi pia uamuzi huo utakuwa umezingatia masuala mengine ambayo
yanafanana na suala hilo na tayari yanaweka precedences. Mathalani hata
sasa vipo vyama ambavyo pamoja na kuwa na uwakilishi bungeni (mbunge
mmoja), ambayo ni sawa na asilimia 0.000 katika bunge la sasa, hata
katika baadhi ya maamuzi yanayozingatia kanuni za namna hiyo au
zinazofanana na hizo, taratibu za kisheria zilizopo zinawaweka kando
katika masuala kadha wa kadha kama ruzuku au kupata wabunge wa viti
maalum. Hiyo inadhihirisha kuwa vyama vikafanye kazi ya siasa kuongeza
viti bungeni ili vipate au kuongeza nafasi za wagombea wa EALA
watakaowakilisha nchi yetu kwenye bunge hilo.
Ni muhimu wakajua kuwa nafasi hizi za EALA kwa utaratibu uliopo sasa
hazigawiwi tu kama sandakarawe au jugu ama pipi. Ni matokeo pia ya kazi
kubwa iliyofanyika wakati wa kampeni uchaguzi uliopita.