Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
leo tarehe 04 Aprili, 2017 amefanya mabadiliko madogo katika safu ya
Makatibu Wakuu.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza
kuwa Mhe. Rais Magufuli amemteua Prof. Kitila Alexander Mkumbo kuwa
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Prof. Kitila Alexander Mkumbo anachukua nafasi ya Mhandisi Mbogo Futakamba ambaye amestaafu.
Kabla ya Uteuzi huu Prof. Kitila Alexander Mkumbo alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Leonard Akwilapo kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Kabla ya Uteuzi huo Dkt. Leonard Akwilapo alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Kufuatia uteuzi huo aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia Bi. Maimuna Tarishi amehamishwa na kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya
Waziri Mkuu (Bunge).
Bi. Maimuna Tarishi anachukua nafasi iliyoachwa na Mussa Uledi ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.
Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Ave Maria Semakafu kuwa Naibu Katibu
Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambako anajaza nafasi
iliyoachwa na Dkt. Leonard Akwilapo ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu
wa Wizara hiyo.
Kabla ya Uteuzi huo Dkt. Ave Maria Semakafu alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).
Wateule hao wataapishwa kesho tarehe 05 Aprili, 2017 saa 3:00 Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
