Katika mahojiano ya kwanza tangu astaafu aliyoyafanya hivi karibuni,
Jaji Othman alitoa mfano wa jinsi Mahakama ilivyoshughulikia kwa haraka
kesi za uchaguzi wa mwaka 2015 uliokuwa na mvutano mkubwa.
Jaji huyo aliyefanya kazi za sheria nje na ndani ya nchi pamoja na
taasisi kadhaa za kimataifa, alieleza kuwa kesi za uchaguzi za ubunge na
udiwani zimemalizika bila malalamiko ya upendeleo.
Hata hivyo, anasema bado mahakama ina changamoto nyingi ikiwamo kila
mkoa kuwa na Mahakama Kuu, kuongeza idadi ya mahakama za mwanzo na
uboreshaji wa miundombinu huku akisikitishwa na baadhi ya mahakama
kutokuwa na umeme.
Jaji Othman ambaye alisoma sheria darasa moja na Waziri Mkuu mstaafu,
Mizengo Pinda, angependa kuona watendaji wa mahakamani wakipambana ili
kuhakikisha wanamaliza kabisa mlundikano wa kesi.
Ukimuliza kitu anachokikumbuka zaidi, Jaji Chande anasema katika
utumishi wake mahakamani hatosahau kesi ya mtoto aliyechunwa ngozi
mkoani Mbeya iliyofikishwa mbele yake.