CHAMA cha Wananchi (CUF) kimemtaka Maalim Seif Sharif Hamad kueleza
ukweli ili jamii ipate kuelewa kinachoendelea ndani ya chama hicho hasa
kuhusu mambo muhimu.
Hayo ni pamoja na suala la nafasi yake ya ukatibu mkuu kukaimiwa, Bodi
ya Wadhamini na kesi nne mahakamani, ambazo Seif na wenzake walifungua.
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa CUF, Magdalena Sakaya jana
ilieleza kwamba anachofanya Maalim Seif na wenzake ni kuwatoa wana CUF
kwenye hoja za kikatiba za kushughulikia mgogoro wa uongozi ndani ya
chama hicho.
Kuhusu suala la kukaimiwa kwa nafasi ya Katibu Mkuu, Sakaya alisema hilo
ni suala la kikatiba na si utashi wake au wafuasi wake.
"Tumeeleza na kunukuu ibara ya 93 kifungu cha 2 mara kadhaa. Kifungu
hiki kinampa madaraka Naibu Katibu Mkuu anayetoka upande wa pili wa
Muungano tofauti na anaotoka Katibu Mkuu, kukaimu nafasi na kutekeleza
majukumu ya Katibu Mkuu mpaka pale Katibu Mkuu atakapokuwa tayari
kutekeleza majukumu yake," ilisema taarifa hiyo ikimnukuu Sakaya.
Alisema anachopaswa kufanya Maalim Seif ni kusema kifungu hicho hakipo
au hakisemi hivyo, ili jamii ipate kuelewa na si kubadilisha maneno.
“Ni kweli CUF tumeandika barua kumjulisha Msajili wa Vyama vya Siasa
kuhusu suala hilo naye amejibu akikiri kupokea barua na ameridhia kwa
mujibu wa Katiba yetu,” alisema.
Alisema Profesa Lipumba na Maalim Seif hakuna kati yao mwenye uwezo wa
kumsimamisha mwenziwe au kuteua mtu wa kukaimu nafasi ya mwenziwe na
kwamba suala la Maalim Seif kuomba kusajili Bodi mpya, na nakala ya
maombi hayo kuyawasilisha Ofisi ya Msajili ni kichekesho kama si
kujichanganya.
"Maalim Seif na genge lake wamefungua kesi Mahakama Kuu ya kutotambua
msimamo na ushauri wa Msajili kuhusu uliokuwa mgogoro wa uongozi ndani
ya CUF na inaitaka Mahakama Kuu itamke kuwa Msajili wa Vyama hana haki
ya kuangalia mambo ya ndani ya CUF.
“Swali kwa Maalim Seif na genge lake, je wanapopeleka nakala ya maombi
ya kusajiliwa Bodi yao Ofisi ya Msajili huko si kuingilia mambo ya ndani
ya vikao vya chama ? Au ndio kusema kwamba sasa Seif na genge lake
wameamua kumtambua Msajili kupitia nyuma ya pazia?”
Aliongeza kuwa lingekuwa jambo jema kama Maalim Seif sasa angekiri wazi
kwamba chama hicho kikatiba hakina Bodi halali kama ambavyo Msajili
alisema kwamba Bodi ya Wadhamini ya CUF ni mfu na haipo kisheria, ndiyo
maana sasa anahangaika kusajili Bodi mpya.
Alihoji kama hivyo ndivyo, je Maalim Seif anaweza kuieleza jamii na wana
CUF kwa ujumla kuwa zile kesi nne mahakamani zilifunguliwa na Bodi ipi
ikiwa hivi sasa yeye anaomba kusajili Bodi mpya? Au ndiyo kusema ameamua
kufuta kesi zote kimyakimya?
Aliongeza kuwa ni vema akasema wazi ikiwa maombi yake ya kufungua Bodi
mpya yatakubalika na kueleza ni ipi sasa itasimamia kesi mahakamani.
"Maalim Seif hajui atendalo kwa sasa, ni vyema amwache Kaimu Katibu Mkuu
Sakaya na Kamati mpya ya Utendaji wasimamie shughuli za chama ikiwamo
ya kuwafanyia kampeni na kuwaombea kura wagombea wetu wa Bunge la Afrika
Mashariki na Kaimu Katibu Mkuu yuko Dodoma akifanya kampeni kwa
wagombea wetu Habib Mnyaa, Thomas Malima na Sonia Magogo,” alisisitiza.
Aliwajulisha wana CUF kokote waliko na Watanzania kwa jumla yao kuwa
chama hicho kiko katika mikono salama ya viongozi wanaojitambua ambao
hawaendeshwi kwa fedha za kifisadi, bali wanaendesha chama kwa mujibu wa
Katiba yake ya mwaka 1992 toleo la 2014.