
Kupitia ukurasa wake wa FaceBook kiongozi huyo ameandika hivi..
Jana nilipokuwa natoa mada kuhusu miaka 50 ya Azimio la Arusha
niliongelea pia suala la umakini wa viongozi katika kauli zao. Kwamba
Kiongozi lazima ujue unatoa kauli gani wakati gani. Niliwaeleza
wanachama na wageni wengine katika mkutano wa ACT Wazalendo kuwa Amri ya
kiholela aliyoitoa Rais John Magufuli kuzuia usafirishaji wa Mchanga wa
Dhahabu imepelekea nchi yetu kupoteza USD 880m Kama kodi ya ongezeko la
Mtaji kutokana na mauzo ya Acacia Mining.
Hivi sasa nchini kwetu kuna sheria ya kutoza 20% ya thamani ya mauzo
iwapo kampuni zinauziana hisa. Tozo inayotozwa inaitwa Capital Gains
Tax. Kodi hii mpya ilitungwa mwaka 2012 ili kukabili wawekezaji
waliokuwa wanauziana makampuni juu Kwa juu bila Tanzania kupata lolote.
Tanzania imeshafaidika na kodi hiyo Kwa mauzo mbali mbali ambayo
yamekwisha fanyika kwenye sekta mbalimbali.
Wakati Rais anatoa AMRI kuhusu Mchanga wa madini kusafirishwa kwenye nje
ya nchi kulikuwa na mazungumzo yanaendelea kati ya Kampuni ya Acacia
mining ( yenye Assets zinazozalisha nchini Tanzania tu kwa sasa -
Buzwagi, Bulyanhulu na North Mara) na kampuni nyengine ya nchini Canada
kuhusu Acacia kununuliwa Kwa USD 4.4bn. Mara baada ya amri hiyo
mazungumzo yalivunjika na hivyo mauzo kutofanyika.
Iwapo Rais angechelewa kutoa kauli yake Kwa wiki moja tu mazungumzo yale
yangepelekea mkataba wa mauzo kusainiwa na hivyo Serikali ingepata 20%
ya thamani ya Mauzo Kama kodi ya Ongezeko la Mtaji ( capital gains tax
). Hivyo kauli ya Rais imesababisha hasara Kwa nchi yenye thamani ya USD
880m sawa sawa na shilingi 1.8 trilioni.
Tafiti zinaonyesha kuwa gharama ya kujenga ' refinery ' ya kuchenjua
dhahabu hapa nchini ni USD 800m. Hivyo mapato ambayo yangepatikana
kutokana na kodi ya mauzo ya Acacia yangewezesha nchi kujenga refinery
na kufikia lengo la Rais la kuwa na uchenjuaji wa mchanga ule hapa hapa
nchini. Rais angetulia angeweza kuua ndege wawili Kwa jiwe moja, 1)
kiwanda cha kuchenjua kingejengwa nchini na 2) mchanga usingesafirishwa
tena kwenda China na Japan.
Hata hivyo Tanzania haina mchanga wa kutosha wa kushibisha hiyo refinery
Kwa mujibu wa teknolojia ya sasa ( soma maelezo yangu hapa chini Kwa
Mhariri wa RaiaMwema). Hivyo Rais angeweza kutumia mapato hayo Kwa
matumizi mengine ya Maendeleo. Kwa mfano Bunge lilitenga kama USD 430m
hivi kujenga Reli ya kisasa na tayari Serikali imeshaingia mkataba na
kampuni kutoka Uturuki kujenga Reli hiyo kipande cha Dar es salaam mpaka
Morogoro. Lakini gharama ya kipande hicho ni USD 1.2bn. Kwahiyo Rais
angeweza kutumia mapato haya ya mauzo ya Acacia kuongezea kwenye kipande
hiki na hivyo kuepuka kukopa kuziba nakisi ya USD 800m iliyopo Sasa na
Bunge kwenye Bajeti ya 2017/18 lingetenga fedha za kuanzia Morogoro
kwenda Dodoma.
Kama Mipango ya Reli ipo sawa, Rais angeweza kutumia fedha za capital
gains tax kutoka Acacia kujenga vyuo vya VETA kila Wilaya na kila Kambi
ya JKT na chenji ingebaki. Tanzania inahitaji tshs 750 bilioni kujenga
vyuo vya VETA kila Halmashauri ya Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji
nchini.
Rais angejifunza kujizuia kutoa matamko barabarani angeisaidia Sana nchi
na kujisaidia yeye mwenyewe kutimiza ndoto zake kwa nchi anayoongoza.
Mimi binafsi naunga mkono kuwa ni lazima tuchenjue dhahabu hapa hapa
nchini badala ya kupeleka mchanga Japan na China. Lakini ni muhimu
maamuzi hayo yawe na ushahidi wa kisayansi badala ya matamko holela
ambayo madhara yake Kwa nchi ni makubwa mno.
Zitto Kabwe, Mb
Arusha
26/3/2017