HATIMAYE. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Paul Makonda kuhojiwa kwa dakika 180 na kamati ya Haki, Maadili
na Madaraka ya Bunge kutokana na kauli aliyoitoa Februari mwaka huu
inayodaiwa kudhalilisha hadhi ya mhimili huo wa Dola.
Makonda akiwa amevaa shati ya maua na suruali nyeusi aliwasili bungeni
jana saa 4 asubuhi kuitikia wito huo uliopitishwa na Bunge Februari 8
mwaka huu, ikiwa zimebaki siku saba tu kabla ya kuanza vikao vya Bunge
la Bajeti.
Siku hiyo ya Februari 8, Bunge lilitumia dakika 45 kupitisha kwa kauli
moja maazimio manne, likiwemo la kuitwa kwa Makonda na mkuu wa wilaya ya
Arumeru, Alexander Mnyeti kutokana na hoja iliyowasilishwa na Mbunge wa
Ukonga, Mwita Waitara akisema wateule hao wa Rais wametoa kauli
zinazodhalilisha Bunge.
Wakati Makonda akisema wakati mwingine wabunge hulala bungeni kwa kukosa
cha kuzungumza, Mnyeti aliandika katika ukurasa wake wa facebook kuwa
wabunge ni wapuuzi kutokana na michango yao wakati walipohoji hatua ya
Ma-DC na Ma-RC kutoa amri za kuwaweka ndani viongozi wa siasa.
Hata hivyo, jana ilikuwa zamu ya mkuu huyo wa mkoa ambaye habari za
ndani kutoka katika kamati hiyo zinaeleza kuwa alikiomba radhi chombo
hicho cha kutunga sharia, baada ya kubanwa kwa maswali ambayo mengine
alishindwa kuyajibu.
Kuhojiwa kwa mteule huyo wa Rais, huenda kukawatuliza baadhi ya wabunge
walionukuliwa katika vyombo mbalimbali vya habari wakieleza kuwa iwapo
Bunge lingeshindwa kumhoji mkuu huyo wa mkoa, moto ungewaka katika vikao
vya Bunge la bajeti.
Hata hivyo, mteule huyo wa Rais bado anaweza kuzua gumzo bungeni
kutokana na kauli na matukio mbalimbali yanayomhusu, likiwamo la kuvamia
kituo cha Clouds ambalo aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo Nape Mnauye aliliundia tume iliyothibitisha Makonda kuvamia
kituo hicho, ambayo hata hivyo yanatajwa kusababisha Nape kuvuliwa
uwaziri.
Jingine ni utata wa elimu ya Makonda na madai ya kughushi na kutumia
vyeti vya kidato cha nne vya mtu mwingine, ambayo mashtaka yake
yamefikishwa Tume ya Maadili ya Viongozi na Meya wa Manispaa ya Ubungo,
Boniface Jacob.
Akizungumza baada mahojiano hayo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, George
Mkuchika alisema, “Leo (jana) tumekutana baada ya kuagizwa na Spika kwa
mujibu wa kanuni za Bunge. Kamati yetu hukutana pale tu inapoagizwa na
Spika.”
“Spika aliagiza kamati yetu imuite makonda ili kumhoji kufuatia azimio
la Bunge lililopitishwa Februari 8. Pamoja ana mambo mengine alitakiwa
kufka mbele ya kamati kujibu tuhuma zinazomkabili.”
Mkuchika alisema kwa mujibu wa azimio hilo, Makonda alidaiwa kutoa kauli
hiyo kupitia kituo cha Televisheni cha Clouds kwamba wabunge
wanasinzia, jambo alilosema kuwa lilionekana kama dharau kwa Bunge.
“Napenda kutoa taarifa kuwa Makonda leo (jana) amekuja mbele ya kamati
na ametupa ushirikiano mzuri, tumepokea maelezo yake na naweza kusema
kuwa kamati imemaliza kazi yake iliyoagizwa,” alisema Mkuchika.