
Rais wa Malawi, Peter Mutharika ameanza tena chokochoko baada ya
kutangaza kuwa hakuna nchi ambayo inamiliki kwa pamoja Ziwa Nyasa na
kwamba haijafikia makubaliano na nchi yoyote, hivyo ameahidi kulinda
umiliki na masilahi yake.
Kauli hiyo ni tofauti na mazungumzo ya Mutharika na Rais John Magufuli
yaliyofanyika Januari 30 jijini Addis Ababa, Ethiopia wakati walipokuwa
wakihudhuria kikao cha Umoja wa Afrika (AU).
Katika taarifa iliyotolewa na Idara ya Mawasiliano ya Rais baada ya
kikao hicho, ilisema marais wote wameridhishwa na jitihada zinazofanywa
na jopo la usuluhishi lililoteuliwa na Umoja wa Maendeleo wa Nchi za
Kusini mwa Afrika (Sadc).
Jopo hilo linaongozwa na rais wa zamani wa Msumbiji, Joachim Chisano.
Mwananchi ilimtafuta Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Dk Augustine Mahiga ili kujua msimamo wa Tanzania lakini
hakupatikana na simu ya Naibu Waziri Dk Susan Kolimba iliita bila
majibu.
Mkuu wa kitengo cha mawasiliano katika wizara hiyo Mindi Kasiga alikiri
kuiona taarifa hiyo ila alisema anayeweza kulizungumzia suala hilo ni
Naibu Waziri.
“Tumeiona hiyo taarifa ila jaribu kumtafuta Naibu Waziri maana Waziri
atakuwa nje ya nchi. Ninachofahamu baraza la usuluhishi bado linaendelea
na vikao vyake. Ukimpata naibu waziri atakuwa na maelezo ya
kina.”alisema Mindi.
Lakini, akihudhuria Siku ya Maji Duniani Jumatano iliyopita mjini
Mangoshi, Rais Mutharika alisisitiza msimamo wa Malawi kulinda umiliki
wa ziwa hilo dhidi ya watu aliowaita wavamizi.
Mutharika alisema Malawi ndiye mmiliki pekee wa Ziwa Malawi, ambalo huku
linajulikana kama Ziwa Nyasa, na kuonya kuwa utawala wake hautavumilia
watu watakaokuwa na nia ya kuyumbisha taarifa za umiliki.
“Hebu tulilinde ziwa letu. Hili ni ziwa letu na ninaposema ziwa letu
namaanisha ziwa lote. Mtu yeyote asifanye kosa la kubadili umiliki ambao
umekuwepo kwa miaka 124 iliyopita,” alisema Mutharika akikaririwa na
tovuti ya Nyasa Times la Malawi juzi wakati wa mkutano huo uliofanyika
ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Nkopola Lakeshore mjini Mangochi.
“Tunathamini ziwa letu na tutahakikisha tunachukua hatua za kulilinda kwa gharama zozote,” alisema.
Mutharika aliwataka wananchi kupunguza matumizi mabaya ya maji ili
yapatikane kwa ajili ya kilimo na viwandani wakati wa msimu wa ukame.
Hivi karibuni, Malawi na Tanzania zimejikuta katika mzozo wa umiliki wa
Ziwa Nyasa lililo kusini mwa Tanzania, mzozo ambao umesababisha kuanza
kwa mazungumzo ya usuluhishi kumaliza kutokubaliana huko baada ya nchi
hizo mbili kushindwa kufikia muafaka. Mzozo wa mpaka kwenye Ziwa Nyasa
umekuwepo tangu mwaka 1967.
Lakini, mzozo wa hivi karibuni umeibuka baada ya Malawi kuanza utafiti wa mafuta na gesi kwenye ziwa hilo.
Hata hivyo, Mutharika alisema uchimbaji mafuta utaendelea katika ziwa
hilo licha ya wanaharakati wa mazingira kuitaka Malawi iache mpango huo.
“Wale wanaohofia kuhusu mipango yetu ya kutafuta na kuchimba mafuta
hawana sababu ya kuhofia. Kama tutaamua kuchimba mafuta katika ziwa,
tutahakikisha tunatumia teknolojia safi,” alisema akikaririwa na Nyasa
Times.
CREDIT - MWANANCHI