SHAHIDI katika kesi inayomkabili mshitakiwa Salum Njwete ‘Scorpion’, ya
kuiba kujeruhi na kumtoboa macho Saidi Mrisho amedai mshitakiwa huyo
ni mlinzi wa amani.
Katika kesi hiyo iliyoendelea kusikilizwa jana kwenye Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, shahidi huyo, Deus Magosa alidai
anamfahamu hivyo mshitakiwa.
Shahidi huyo mkazi wa Buguruni ambaye ni kiongozi wa ulinzi shirikishi
wa eneo hilo, alidai kuwa yeye ndiye aliyempa ajira ya ulinzi wa amani
mshitakiwa kwenye eneo hilo la biashara ndogondogo.
Mwendesha mashitaka wa Serikali, Nassoro Katuga alimhoji shahidi huyo
namna anavyomfahamu Scorpion ambapo mbele ya Hakimu Flora Haule, Magosa
(46) alijibu anamfahamu kwani mshitakiwa aliajiriwa na wafanyabiashara
wadogo kuwalinda pamoja na biashara zao pamoja na uongozi wao wa ulinzi
ushirikishi.
Aliendelea kudai kuwa Salum alikuwa akilipwa Sh 10,000 kwa siku na
wafanyabiashara hao kwa kuwawezesha kuendelea na biashara zao bila
matukio ya wizi.
Hata hivyo, shahidi huyo alipoulizwa kama anakumbuka kilichotokea
Septemba 6 mwaka jana, Magosa alijibu kwamba siku hiyo hakuwapo alikuwa
msibani nje ya Dar es Salaam
Aliendelea kudai kuwa aliporudi alisikia watu wakizungumza mtaani,
kwamba kuna mtu alitobolewa macho na kujeruhiwa katika tukio lililotokea
maeneo ya Buguruni ambapo walimtaja mshitakiwa kuwa ndiye aliyehusika
na tukio hilo.
Wakili alimwuliza baada ya hapo nini kiliendelea shahidi akajibu
waliitwa Polisi na alipokwenda aliulizwa kama anamfahamu Salum Njwete
ambapo alijibu anamfahamu na kumtaka akamwite.
Shahidi alidai alimfuata mshitakiwa na bila shaka wala kukataa alisema
yeye ni raia mwema na alikwenda polisi bila kukamatwa na akaambiwa
niondoke akamwacha mshitakiwa Polisi Buguruni.
Wakili Katuga alisema kesi hiyo itaendelea kusikilizwa Aprili 18 ushahidi utakapoendelea kutolewa.
