Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, Suleiman Kova
amesema marafiki wengi wa viongozi si marafiki wa kweli bali ni
marafiki wa zile nafasi walizonazo.
Kamanda Kova alisema hayo katika uzinduzi wa Chuo Cha Fursa (APEC)
kilichopo maeneo ya Ukonga, mwishoni mwa wiki ambapo mkurugenzi wa chuo
hicho alimualika kuhudhuria hafla hiyo.
“Mkurugenzi wa APEC, Respicius Timanywa, alikuja ofisini kwangu mwaka
2010 akitaka ushauri na kupata maelekezo kuhusu mtaala wa kufundishia
bodaboda, tuliandaa pamoja naye, leo amenikumbuka kanialika katika
uzinduzi wa chuo,” alisema Kamanda Kova.
Aliongeza “Ni watu wachache sana wanaoweza kukumbuka, wengi ni marafiki
wa kiti chako sio wewe, ukitoka katika kiti ukimpigia simu hapokei na
mwingine anaitika kisha anazima kabisa.”
Aidha Kamanda huyo alisema kwa sasa anajishughulisha na kutoa ushauri wa masuala ya maafa, majanga na uokoaji.